Dalili za IBD ni gani?

Dalili za Ugonjwa wa uvimbe wa Tumbo ni tofauti; ugonjwa unaweza kuanza kwa ghafla au kukua polepole baada ya muda.

Kuendesha

Kuendesha katika IBD ni tofauti na kuendesha kunakohusishwa na hali ya kawaida kama vile ugonjwa wa tumbo (maambukizi ya virusi au bakteria) au sumu ya chakula ambayo watu wengi wamepitia kwa wakati fulani, au kuendesha kunakosababishwa na ugonjwa mkali wa matumbo. Wakati mwingine,kuendesha katika IBD hudumu kwa wiki au miezi, huku mara nyingine ikipungua. Kuendesha kunaweza kutokea kwa hamu kubwa kiasi kwamba mtu hawezi kufika msalani kwa wakati (kutoweza kujizuia). Pia kunaweza kuwa na damu, kamasi au usaha. Kuendesha kunakoamsha mtu mara kwa mara kutoka kwa usingizi inaweza kuwa ishara nyingine ya IBD.

Maumivu ya kichomi ndani ya tumbo

Haya yanaweza kuwa makali sana na mara nyingi hutokea baada ya kula au kabla ya kutoa kinyesi.

Uchovu mwingi

Hii inaweza kutokana na ugonjwa wenyewe, kutokana na upungufu wa damu (ukosefu wa damu) au ukosefu wa usingizi kwa sababu ya maumivu au kuendesha.

Joto mwilini

Joto la kiwango cha chini inaweza kuwa ishara ya IBD.

Kupoteza hamu ya kula na kupoteza uzito.

Kupunguza uzito kunaweza kusababishwa na mwili kutochukua virutubisho kutoka kwa chakula unachokula kwa sababu ya uvimbe kwenye utumbo.

Baadhi ya watu wenye IBD, hasa Crohn, wanaweza kupata matatizo, ikiwa ni pamoja na:

Makovu

Huu ni wakati ambapo kuna uvimbe unaoendelea na kisha upone na kusababisha kovu. Hii inaweza kuunda sehemu nyembamba ya matumbo, inayoitwa ukali, ambayo inaweza kusababisha kuziba kwa utumbo au koloni.

Fistula

Hizi hutokea sana kwa watu walio na ugonjwa wa Crohn. Fistula ni njia isiyo ya kawaida au njia ya kupita inayosababishwa wakati ugonjwa wa Crohn “unapochimba” kupitia utando wa utumbo au koloni. Kwa walio na ugonjwa wa Crohn, fistula hutokea karibu na njia ya haja kubwa (fistula ya pembeni mwa mkundu) na kusababisha uvimbe au jipu chungu ambalo linaweza kutoa kamasi, usaha au kinyesi. Fistula pia inaweza kutoka kwenye ngozi (fistula ya ngozi) au kuunganisha kitanzi kimoja cha utumbo na kingine (fistula ya ndani).

Wakati mwingine, IBD inaweza kuathiri sehemu zingine za mwili. Hizi zinaitwa udhihirifu wa IBD wa nje ya matumbo ambao hujumuisha:

Maumivu ya viungo

Kuvimba kwa viungo, au ugonjwa wa yabisi, inamaanisha kuwa maji yamejikusanya kwenye nafasi ya viungo na kusababisha uvimbe wenye uchungu. Mara nyingi huathiri viungo vikubwa vya mikono na miguu, ikiwa ni pamoja na viwiko, mikono, magoti na vifundoni.

Maumivu katika sehemu ya chini ya mgongo

IBD inaweza kusababusha kuvimba kwa sehemu ya chini ya mgongo na nyonga, hali inayoitwa “ankylosing spondylitis”. Hali hii husababisha maumivu na ugumu kwenye sehemu ya chini ya mgongo.

Kuvimba kwa macho

Wagonjwa wa IBD mara nyingi huadhirika na hali inayojulikana kama “episcleritis”, ambayo huathiri safu ya tishu inayofunika sehemu nyeupe ya nje ya jicho, na kuifanya kuwa nyekundu, yenye maumivu na kuvimba.

Matatizo ya ngozi

Kuna matatizo kadhaa ya ngozi yanahusishwa na IBD ambayo yanajumuisha matuta mekundu yenye uchungu kwenye sehemu ya chini ya miguu (erythema nodosum) na vidonda vya ngozi vyenye maumivu (pyoderma gangrensum).